Hivi uliwahi kujiuliza hivi ni kwanini baadhi ya mahusiano ya kimapenzi hufa mapema, kama si kufa basi kushuka kwa mahusiano hayo? Moja kati ya sababu ambayo husababaisha kufa kwa mahusiano ni ile tabia ya kuchokana mapema katika mahusiano na moja kati ya sababu kubwa ambayo hupelekea kuchokana mapema ni:
1. Mazungumzo
Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha , aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana. Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake.
Kwa mfano: Mwanamke ambaye kila anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu wakati wote.
Mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.
2. Kuzoeana
kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususan kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla.
Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana, kwa mfano: siku za utoto wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu, mapokezi yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini.
Lakini baada ya kuzoeana yote hayo hubadilika, mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumuonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku, mambo ya Hinna, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini na sio nyumbani. Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau.