Thursday, February 21, 2019

Tabia 10 za watu waliojipanga katika kufanikiwa

Tabia 10 za watu waliojipanga katika kufanikiwa

Kuna watu ukitazama utendaji wao wa kazi au maisha yao yanavutia. Ukitazama jinsi wanavyotekeleza mambo yao unaweza kufikiri kuna mfumo fulani unawaendesha au kuwaongoza kwa siri.

Mara nyingi watu hawa huwa na mfuatano au mpangilio mzuri na unaoeleweka wa kazi au maamuzi yao. Kwa kifupi watu hawa hufanikiwa sana na ndiyo huitwa watu waliojipanga.

Inawezekana nawe unahitaji kufahamu sifa za watu waliojipanga ili ujifunze jambo. Basi karibu nikushirikishe tabia 10 za watu waliojipanga.

1. Wanaandika kila kitu.
Kuandika vitu ni njia mojawapo ya kutekeleza mambo kwa mpangilio. Watu waliojipanga huandika mambo yote wanayotakiwa kufanya ili wasiyasahau na wanyafanye kwa wakati.

Watu waliojipanga hukagua pale walipoandika mara kwa mara ili kuona wamekamilisha lipi na lipi bado hawajakamilisha.

2. Wanaweka kila kitu mahali pake
Unapoweka kila kitu mahali pake, ni wazi kuwa ofisi au nyumba yako itaonekana imejipanga. Watu waliojipanga huweka kila kitu mahali pake; hivyo hawapotezi muda wa kutenga siku ya kupangilia nyumba au ofisi.

Kwa mfano kama umeanua nguo, basi usizitupe kwenye kochi au kitandani bali zikunje au uzitundike. Unapomaliza kula pia usiache vyombo mezani bali vioshe uvihifadhi badala ya kuviacha mezani au kuvitelekeza jikoni. Ukizingatia kuweka kila kitu mahali pake utakuwa mtu aliyejipanga zaidi.

3. Wanagawa majukumu
Watu waliojipanga hawajitutumui kufanya kila kitu; watu hawa hugawa majuku kwa watu stahiki. Badala ya kufanya kila kazi kwa ufanisi mdogo, ni vema ukagawa kazi hizo kwa watu wengine.

Kwa mfano ikiwa ni kwenye ngazi ya familia, mtoto mmoja anaweza kufagia, mwingine akadeki na wewe ukapika au kufanya shuguli nyingine muhimu.

4. Wanapanga kesho leo.
“Maandalizi mazuri ya kesho hufanywa leo.”

Watu waliojipanga wanafahamu kuwa kesho haiandaliwi kesho bali leo. Hivyo hubainisha mapema majukumu wanayotakiwa kuyatekeleza kesho kwa kutegemea vipaumbele vyake.

Unapopanga kesho leo hukufanya kuwa na maandalizi mazuri na kuepuka kufanya mambo bila kuzingatia umuhimu wake.

5. Wanafanya kazi kwa bidii
Watu waliojipanga hufanya kazi kwa bidii ili wasije wakavuruga utaratibu au mpangilio wao. Hili ni kinyume kwa watu wasiojipanga kwani wao huahirisha mambo wakidhani kuwa wana muda mwingine.

Kwa kufanya kazi kwa bidii kunakufanya uwe na ratiba nzuri na inayoeleweka ambayo haiingiliwi na madeni ya kazi zilizoahirishwa.

6. Wana ratiba na wanaifuata
Tabia moja wapo ya watu ambao hawajajipanga ni kukosa ratiba, wao huamka na kufanya lile linalokuja mbele yao; au wakiwa na ratiba basi ni vigumu sana wao kuifuata.

Watu waliojipanga wana ratiba nzuri tena wanayohakikisha wanaifuata vyema. Ikiwa mtu aliyejipanga anatakiwa kuwa mahali au kukamilisha jambo fulani kwa wakati fulani basi hufanya hivyo bila kuacha.

7. Wana vipaumbele
Watu waliojipanga wanafahamu ni nini cha muhimu zaidi kwenye maisha yao. Kwa kufahamu hili watu hawa huweza kuvipa vitu nafasi kulingana na umuhimu wake.

Watu wasiojipanga wanaweza kuangalia filamu (movies) au kukaa kwenye mitandao ya kijamii huku wakiacha majukumu yao ya msingi ya kila siku.

8. Wanajali afya zao
Hakuna mafanikio au ufanisi katika jambo lolote kama hakuna afya nzuri. Watu waliojipanga wanafahamu wazi kuwa afya njema itawawezesha kufanya majukumu yao vyema, hivyo wanajali afya zao.

Ni wazi kuwa mtu anapougua majukumu au ratiba zake nyingi huvurugika au kukwama; hivyo kwa kulinda afya yako utaweza kutimiza majukumu yako kwa mpangilio uliojiwekea.

9. Wanajiandaa kwa dharura
Dharura zipo kila mara kwenye maisha, na mara nyingi ndizo huvuruga ratiba za watu. Utasikia kauli kama vile nimepata dharura sitoweza kuja, nimepata dharura ndio maana sikumaliza, kuna kitu kilijitokeza, n.k.

Kwa hakika watu waliojipanga hujiandaa kwa dharura ili zisije zikavuruga mpangilio wao mzuri waliojiwekea.

10. Wanajali muda
Kama nilivyoeleza kwenye hoja zilizopita, watu waliojipanga hawakubali kupoteza muda kwani kila muda wao una jukumu fulani kwenye ratiba.

Watu waliojipanga huamka mapema na huepuka tabia au matendo ambayo kimsingi yanapoteza muda.

Hali hii ni kinyume kwa watu wasiojipanga, kwani wao huchelewa kila mahali au hutumia muda wa msingi kwenye mambo yasiyo na tija.

Kwa hakika mfumo wa maisha wa watu waliojipanga ni mzuri na wenye manufaa makubwa kwa yeyote yule anayetaka kufikia malengo. Kwa ufupi tunaweza kusema matumizi mabaya ya muda ndiyo tofauti kubwa kati ya watu waliojipanga na wale wasiojipanga.