Nini hutokea mwilini wakati wa mzunguko wa hedhi?
Mzunguko wa hedhi huendeshwa na homoni mbalimbali za mwili. Wakati wa mzunguko wa hedhi, sehemu za kwenye ubongo ziitwazo ‘hypothalamus’ na ‘pituitary gland’ hupeleka taarifa za homoni kwenda kwenye ovari na kurudi kwenye ubongo. Taarifa hizi huziweka ovari na mfuko wa uzazi tayari kwa ajili ya kubeba mimba.
Kwanza pituitary gland hutoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone-FSH ambayo huenda kusababisha kukomaa kwa yai ndani ya ovari. Baada ya hapo homoni ya estrogen hutolewa ambayo huenda kusaidia ujenzi wa ukuta wa mfuko wa uzazi kwa ajili ya maandalizi ya mimba inayoweza kutokea (kwenye ukuta huu ndipo mimba hujishika, kupata virutubisho na kukua).
Wakati kiwango cha estrogen kimepanda mwilini, hali hii husababisha utolewaji wa homoni nyingine iitwayo Gonadotropin-Releasing Hormaone-GnRH kutoka kwenye sehemu ya ubongo.
Uwepo wa homoni ya GnRH husababisha pituitary gland kusababisha ongezeko la homoni ya lutenizing (LH). Baadaye LH husababisha uachiliwaji wa yai kutoka kwenye ovari, kitendo kinachojulikana kitaalamu kama ‘ovulation’.
Baada ya yai kutolewa kutoka kwenye ovari, husogezwa karibu na mfuko wa uzazi ‘uterus’ kusubiri kuungana na mbegu za mwanamme, na endapo litakutana nazo basi mimba hutungwa. Kama hakutatokea muunganiko kati ya yai na mbegu (kitaalamu huitwa ‘fertilization’) basi yai humeguka na kufa ndani ya masaa 6 hadi 24.