Friday, December 28, 2018

Dalili za yai kutoka/kuachiliwa.

Dalili za yai kutoka/kuachiliwa

Muda mfupi kabla ya yai kuachiliwa kutoka kwenye ovari mwanamke hutokwa na ute katika mlango wa uzazi ambao huwa katika hali ya kuteleza na usio na rangi; ni kama sehemu ya nje ya yai bichi (isiyokuwa kiini).

Ute huu huvutika sana pia. Mwanamke anapokuwa katika hali hii huweza kupata ujauzito iwapo atagusana na mbegu za kiume. Ute huu husaidia kurutubisha mbegu za kiume pindi zinaposafiri kupita mlango wa uzazi ‘cervix’.

Iwapo mwanamke hayupo katika kipindi hiki cha yai kuachiliwa, ute wa kwenye mlango wa uzazi ‘cervical mucus’ huwa na rangi tofauti na katika hali ya tofauti.

Ute huu huweza kuwa unanata, mweupe kama maziwa, ukiwa na muonekano kama losheni ya kujipaka au kuwa na rangi ya njano. Ute huu huwa hauvutiki na huwa na harufu kali kidogo.

Aidha, nafasi ya mlango wa uzazi nayo hubadilika wakati wote wa mzunguko wa hedhi. Wakati wa yai kuachiliwa kutoka kwenye ovari, mlango wa uzazi husogea juu kidogo na njia hutanuka kidogo zaidi. Baadhi ya wanawake huhisi hali ya maumivu wakati wa yai kuachiliwa.

Maumivu haya hutofautiana na huweza kuwa ya kuvuta au ya jumla katika sehemu ya tumbo, au maumivu ya kukata upande mmoja wa tumbo ambao ndio yai huachiliwa.