Mbinu za kukabiliana na wivu wa kupitiliza kwenye mapenzi
Wapenzi ambayo wanaopendana hawaoneani wivu, ni sawa na mboga iliyokosa chumvi, hata kama imepikwa vizuri kiasi gani, haitakuwa na ladha nzuri mdomoni.
Vilevile chumvi inapozidi kwenye mboga, ipo wazi kwamba hata kama imepikwa vizuri kiasi gani, haitalika. Kama tunakubal¬iana katika dhana hii, ni vizuri tukakubaliana kwamba wivu ni hisia muhimu katika mapenzi lakini unapozidi, huweza kuwa na madhara makubwa kwa wapendanao.
Upo ushahidi wa matukio mengi ya kutisha katika mapenzi, ambayo yamefanywa kwa sababu ya wivu.
Ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya wivu wa kimapenzi! Wapo walioyakatisha maisha ya wenzi wao, wapo waliowajeruhi vibaya wapenzi wao, wapo waliopigana na kuumizana vibaya na watu wengine kisa kikiwa ni wivu wa mapenzi.
Wapo watu wengi tu wanaoendelea kusota kwenye kuta za magereza kwa sababu ya wivu wa kimapenzi. Bila shaka hata wewe msomaji wangu kichwani mwako unazo kumbukumbu za matukio mengi, mabaya yaliyokutokea wewe au yaliyowatokea watu unaowajua, kisa kikiwa ni wivu wa mapenzi.
Ushahidi huu unaonyesha kwamba kumbe wivu wa kimapenzi si hisia za kawaida zinazopaswa kupuuzwa kwani madhara yake ni makubwa, kwa hiyo ni vizuri kila mmoja akajua namna ya kuudhibiti wivu au namna ya kuishi kwa amani na mtu mwenye wivu uliopitiliza.
Ni ukweli usiopingika kwamba, mtu hawezi kukuonea wivu kama hakupendi ni hii ni pande zote mbili. Ukiona mwenzi wako anaondoka nyumbani, anachelewa kurudi, hujui alipo na wala hujishughulishi naye, ujue kuna walakini kwenye mapenzi yenu.
Ukiona mwenzi wako yuko bize na simu yake mpaka usiku, hujui anachati na nani au anaon¬gea na nani na hutaki kabisa kujishughulisha naye, moyo haukuumi wala hujisikii vibaya, ujue kuna walakini katika penzi lenu.
Hisia za mapenzi zinapokolea , zina kawaida ya kuwafanya wahusika waoneane wivu, yaani hata mwanamke akitoka kwenda dukani, akachelewa kurudi, lazima huku nyuma mwanaume kiroho kiwe kinamdunda, moyoni anawaza ‘pengine amesimamishwa na njemba mwingine anamtongoza’!
Hali kadhalika kwa mwanamke, mumewe akirudi jioni atataka kujua siku yake imekuwaje, amekutana na nani, amezungumza na nani kwenye simu, ametumiana meseji na nani na mambo mengine! Ni wivu wa kimapenzi ndiyo unaomsukuma kufanya hivyo.
Uchunguzi wa saikolojia ya mapenzi unaonyesha kwamba mtu ambaye anamuonea wivu sana mpenzi wake, anayeonewa wivu akijua mbinu sahihi za kumtuliza, uhusiano huo utadumu milele. Hata hivyo, anayeonewa wivu akishindwa kujua mbinu za kushughulikia tatizo hilo, uhusiano huo hauwezi kufika popote na kitakachotokea, ni maafa na madhara makubwa.
Kwa matokeo hayo ya uchunguzi, ni muhimu sana kwa kila mmoja kujua namna ya kumsaidia mwenzi wake mwenye wivu mkali, au kujua mwenyewe namna ya kujidhibiti pale anaposhikwa na wivu mkali unaoamsha hasira za maangamizi. Ni rahisi kukabiliana na wivu endapo utayajua mambo machache ya muhimu kuhusu wivu.