Huu ndiyo udhaifu wa wanaume kwenye mapenzi
NI matumaini yangu kwamba msomaji wangu unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku. Ni Ijumaa nyingine nzuri tunapokutana katika uwanja wetu huu mzuri, kujuzana na kujadiliana kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi.Leo nataka tujadiliane kitu tofauti kidogo ambacho huenda watu wengi hawakijui. Kama wewe ni mwanaume, hivi umewahi kujiuliza unahitaji nini zaidi kutoka kwa mkeo? Kama wewe ni mwanamke, umewahi kujiuliza mumeo anahitaji nini zaidi kutoka kwako ili atulie? Yawezekana likawa ni swali ambalo unaweza kulitafsiri kwamba halina maana lakini majibu yake ni mapana zaidi.
Wengi huwa wanafikiri hitaji kubwa la mwanaume kwa mwanamke, ni kufanya mapenzi na huenda hata wewe ungenijibu hivyo lakini je, hilo ndiyo jibu sahihi? Ipo wazi kwamba tendo la ndoa ndiyo linaloikamilisha ndoa yoyote, iwe imefungwa Kikristo, Kiislam, kimila au kiserikali.
Hakuna ndoa ambayo inaweza kukamilika bila wanandoa kukutana kimwili, hakuna ubishi katika hili lakini je, hilo ndiyo hitaji pekee linaloweza kumfanya mumeo akaridhika na wewe?
Wanawake wengi, hasa wasichana wanaoanza kuingia kwenye ulimwengu wa mapenzi, huhisi kwa sababu wao ni warembo, wana mvuto machoni mwa wanaume au wana maumbo mazuri, basi hiyo ndiyo tiketi ya moja kwa moja ya wao kuolewa na wanaume wazuri na kudumu kwenye ndoa zao.
Hata hivyo, wanapoingia kwenye ndoa, wanakutana na hali tofauti kabisa kiasi cha wengine kujuta kwa nini wameolewa. Kinachowafanya wajute ni kwamba wameingia kwenye ndoa wakiwa hawaelewi wanaume wanahitaji nini zaidi kutoka kwao.
Kwa kutofahamu huko, huelekeza nguvu zao nyingi kwenye tendo la ndoa lakini mwisho hugundua kwamba kumbe tendo la ndoa siyo kitu pekee kinachoweza kuwafanya waume zao wakawapenda na kuwathamini.
Hali ni tofauti kwa wanaume wasiooa ambao kwao, ipo wazi kwamba hitaji lao la kwanza kwa wanawake, huwa ni ngono na wakishakidhi haja zao, huwa hawana tena mpango. Kwa hiyo, tukubaliane kwamba mwanaume akishakuoa na kukuweka ndani, hitaji lake kubwa siyo tendo la ndoa pekee.
Sasa kama ni hivyo, kumbe wanaume huwa wanahitaji nini kutoka kwa wake zao? Winston Parker, ni mshauri na mtaalamu wa mapenzi na uhusiano kutoka nchini Marekani, katika kitabu chake cha What a Man Needs From a Woman, anaeleza kuwa jambo kubwa ambalo wanaume wanahitaji, ni utiifu kutoka kwa wake zao.
Anaeleza kwamba udhaifu mkubwa wa wanaume, ni kuona wanasikilizwa na kupewa utii kutoka kwa wake zao na kudekezwa kama watoto. Hata kama mwanaume alikuwa ‘mtata’ kiasi gani, anapokutana na mwanamke anayemheshimu, kumsikiliza, kumtii na kumdekeza, ni lazima atazama kwenye penzi lake hata kama si mzuri wa sura wala umbo kiasi cha watu wengine kuanza kuulizana ‘anampendea nini yule’?
Ipo kasumba ya wanawake wengi siku hizi, kudai usawa hata katika mambo ambayo hayahitaji usawa. Mwanamke anakuwa jeuri, mkaidi na hamheshimu kabisa mumewe, akikatazwa kufanya jambo fulani anaona kama anatawaliwa, anafanya hata kama anajua mumewe hapendi, kisa ‘haki sawa’.
Matokeo yake, mwanaume wa aina hii akikutana na mwanamke anayemsikiliza na kumheshimu, hata kama ni hausigeli wake, yupo tayari kumkabidhi moyo wake na kumuonyesha mapenzi ya dhati.
Huenda hii ni miongoni mwa sababu zinazowafanya mahausigeli wengi kupindua ndoa za mabosi wao.
Sihalalishi kwamba kama mwanamke ana udhaifu huu basi aadhibiwe kwa usaliti, hapana. Wengine wanakuwa na tabia hizi kwa sababu ya malezi waliyolelewa lakini kama wakieleweshwa kwa upole, huweza kubadilika.