Zifahamu mbinu bora katika malezi
Wazazi wengi bado wanaona aibu kuwa wazi kutoa baadhi ya taarifa na msimamo yao kwa watoto wao wakidhani kuwa muda bado, na ni aibu kufanya hivyo mapema, kumbe jinsi wanavyochelewa ndivyo jinsi ulimwengu unawapa taarifa potofu juu ya vitu kama mahusiano, mapenzi, ngono, ukimwi na magonjwa ya zinaa nk. Mambo haya mengi na tofauti hizi nyingi zinachangiwa na jinsi watoto hawa wanayolelewa na mbinu za malezi ambazo wazazi wamekuwa wakizitumia. Maranyingi nimekuwa nikisema kuwa suala sio mzazi au wazazi kulazimisha watoto kuwa na nidhamu, suala ni njia au mbinu gani za kujenga nidhamu zinatumika. Wengi wamewaharibu watoto wao wenyewe pasipo kujua na wakati huo wao wakidhani wanawajenga na kuwaadabisha.
Mtiririko huu wa aina za malezi utakusadia kujitambua na ikiwezekana kubadilika, kama wewe ni mlezi sasa itakusaidia kubadilisha mtazamo wako kuhusu malezi na kama sio mlezi basi itakuandaa vema kwa mlezi bora baadae. Nia ya mbinu hizi za malezi ni kurekebisha au kujenga tabia za watoto na kuwaelekeza katika muelekeo fulani. Tatizo ni kwamba yako makosa mengi katika malezi yanayofanywa na wazazi na badala yake kuleta uharibifu kwa tabia za watoto wao.
Aina za malezi
Wazazi wanaolea kiamri (Authoritarians)
Hawa ni wazazi wanao lazimisha kwa watoto wao utii, nidhamu na kufuata sheria bila kujali sheria hizo au masharti hayo yako sawa au la. Wazazi wajinsi hii hutoa masharti makali katika kila kitu, mjadala au maswali juu ya kilichosemwa huruhusiwa kidogo sana au maranyingine hukatazwa kabisa. Mtoto au yule anayeadabishwa hukosolewa sana katika kila kitu. Maelekezo ya jinsi ya kuwa na nidhamu hutolewa, kwa mfano, jinsi ya kukaa mezani wakati wa kula, jinsi ya kujiheshimu mgeni au wageni wakiwepo, namna ya kusalimu wakubwa nk. Baadhi ya sheria hizi husisitizwa kwa adhabu, watoto wanafahamu kabisa, kama asipofanya usafi, basi ajiandae kutokula chakula au kuchapwa fimbo.
Wazazi wenyekuruhusu ukaribu (Permissive)
Hawa ni azazi wenye urahisi katika kuingilika, au kukaribiwa na watoto, wazazi hawa huwa na sheria chache sana, mara chache pia huadhibu watoto, hasa pale inapowalazimu. Anayeadhibiwa hupewa heshima yake na kusikilizwa pia.
Wazazi wenye malezi ya kiutawala (Authoritative)
Hawa ni wazazi wenye amri na maarifa katika kusimamia amri zao, mzazi wa aina hii huamini katika kusimama kama mtawala kwa wale anaowaongoza, kwa mfano watoto wake. Hutoa maelezo mazuri na ya kutosha juu ya amri na masharti yaliyoweka na mjadala au maswali huruhusiwa. Mtoto anaruhusa na uhuru wa kuelezea mawazo yake au mtazamo wake katika jambo fulani na hivyo kuweza kushawishi kubadili baadhi ya utekelezaji wa amri au masharti fulani kwa kutumia nguvu ya hoja.
Watoto hupewa nafasi ya kujiona washiriki katika utekelezaji wa masharti au amri zilizowekwa, katika hili watoto huweza kuziangalia amri za nyumbani kama “amri zetu” na sio “amri za baba au amri za mama”. Wanaona pia manufaa au umuhimu wa kuzifuata amri hizo. Adhabu za kuumiza mwili kama vile kuchapwa au kufinywa hutumika kidogo sana, adhabu hizi na adhabu nyingine pia hutumika kwa upendo na sio chuki. Anayeadhibiwa hapa huona dhahiri kuwa anastahili kupokea adhabu na sio kuwa hapendwi au aheshimiki.