Maswali 10 muhimu ya kujiuliza kabla ya kuacha kazi
Wakati wengine wakitafuta kazi usiku na mchana, wengine wanatamani kuacha kazi mara moja. Kutokana na sababu mbalimbali, swala la kuacha kazi linawakabili watu wengi.
Mazingira mabaya ya kazi, matatizo ya kifamilia au kiafya yamekuwa chanzo kikubwa cha watu kutamani au kutaka kuacha kazi.
Swala la kuacha kazi ni swala nyeti ambalo linahitaji utulivu na maamuzi yenye kuhusisha utafiti na busara kubwa. Wengi huacha kazi kutokana na misukosuko midogo na kujikuta wakiingia kwenye matatizo makubwa zaidi.
Ikiwa unataka kuacha kazi unayoifanya ili utafute nyingine au ujiajiri mwenyewe, basi jiulize maswali haya 10 kabla ya kumpungia mwajiri wako mkono.
1. Je unaacha kwa sababu sahihi?
Inawezekana umekaripiwa na mwajiri wako kutokana na kosa ulilolifanya, swala hili limekukasirisha kiasi cha kutaka kuacha kazi. Je kweli madhara ya kuacha kazi ni madogo kuliko yale ya kukaripiwa?
Hakikisha unatafakari kwa kina sababu inayokufanya uache kazi. Usiache kazi kwa mambo madogo ambayo ungeweza kuvumilia yakapita.
2. Je ni wakati sahihi?
Kufanya jambo lolote nje ya wakati ni kosa kubwa. Hakikisha uamuzi unaoufanya wa kuacha kazi ni kwa wakati sahihi.
Wakati sahihi hutegemea maandalizi ya maisha baada ya kuacha kazi; ikiwa bado hujajiandaa au kuna mambo yatakayoharibika kutokana na wewe kuacha kazi, basi subiri kwanza.
3. Chanzo kingine cha kipato ni kipi?
Inawezekana kazi unayotaka kuiacha ndiyo chanzo chako cha kipato. Je utapata wapi fedha kwa ajili ya matumizi yako wakati utakapokuwa umeacha kazi?
Nimeshuhudia watu wakiomba kurudi kwenye kazi zao za zamani kutokana na kutokujiandaa katika eneo la kipato. Hivyo hakikisha una chanzo kingine cha uhakika cha kipato kabla ya kuacha kazi.
4. Je uko kwenye tasnia gani?
Inawezekana unalenga kutafuta kazi sehemu nyingine baada ya kuacha kazi; je tasnia au uwanja unaoufanyia kazi ukoje? Je kuna watu wengi sana? Je uwezo wako katika tasnia ukoje?
Kuacha kazi bila kufikiri juu ya maswala haya kunaweza kukufanya usipate kazi tena. Inawezekana wapo watu tele wanaotafuta kazi kama yako, hivyo kuiacha ni kuipoteza daima.
5. Je utapata kazi nyingine au utafanya nini?
Usiache kazi kabla ya kufahamu kama utapata kazi nyingine au utafanya nini. Hakikisha unafahamu kazi utakayoifanya au kama utajiajiri mwenyewe uwe tayari umeshaweka mikakati sahihi.
Kuacha kazi bila kujiuliza swali hili kutakuweka kwenye hali ngumu.
6. Je utapata stahiki au haki zako?
Kuna stahiki ambazo mtu anazipata mara amalizapo utumishi wake kwa mujibu wa sheria. Je ikiwa utaacha kazi utapata stahiki zako kama vile mafao ya uzeeni?
Hakikisha huachi kazi katika mazingira yatakayokusababisha upoteze mishahara au mafao yako ambayo ungepaswa kulipwa.
7. Je familia inakubaliana na msimamo wako?
Ikiwa una familia ni muhimu ukawashirikisha juu ya uamuzi wako wa kuacha kazi ili nao watoe msimamo wao.
Kuacha kazi bila kushirikisha familia kunaweza kukuweka katika mgogoro au sitofahamu kubwa kati yako na familia yako. Je familia ilikuwa inategemea kazi yako? Je kipato cha familia kitakuwaje? Je watakuwezesha vipi utakapokuwa huna kazi?
8. Je walioamua mamuzi kama yako wakoje?
“Ningejua huja mwishoni.”
Wengi huacha kazi wakidhani mambo yatakuwa rahisi, baada ya kuacha kazi hujikuta wakiwa kwenye hali ngumu.
Chukua muda uwatumie watu wengine walioacha kazi kama shule yako ya kujifunza. Je maisha yao yakoje? Yamekuwa mazuri au mabaya? Tafakari vyema kabla ya kuchukua hatua.
9. Je una akiba ya kutosha?
Akiba ni muhimu kwa ajili ya kukusaidia wakati ambao huna kipato kwa ajili ya kutunza mahitaji yako. Hakikisha umebainisha matumizi yako ya fedha na kuhakikisha unaweza kuyakidhi kwa akiba uliyo nayo.
Usiache kazi bila kuwa na kiasi cha uhakika cha akiba itakayokusaidia wewe na wale wanaokutegemea.
10. Je unaweza kuruhusiwa kurudi kazini?
Kuna wakati mtu anajutia uamuzi wake. Hakikisha kabla ya kuacha kazi umefahamu kama unaweza kuruhusiwa kurudi kazini ikiwa mambo yatakwenda vibaya.
Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa huachi kazi kwa shari bali unaacha kwa amani ili ukitaka kurudi ufikiriwe. Kumbuka! Unaweza pia kuomba likizo ndefu isiyokuwa na malipo (secondment) badala ya kuacha kazi kabisa.