Jinsi gani ya kuwa mzazi/mlezi bora
Wote tutakubaliana na ukweli kwamba malezi ya watoto sio kazi rahisi kama wengine wanavyoichukulia. Malezi ya watoto ni jukumu ambalo twaweza kulibeba vyovyote tunavyotaka lakini tunapokuwa watu wazima au wazee tunafikia kujivunia jukumu hilo au kujilaumu kwa kushindwa kuwa wazazi au walezi bora. Nia yangu katika hili ni kujaribu kuchambua vitu vitakavyo kusaidia na kukuwezesha kuja kujivunia utakapo waangalia wale uliowalea na kuwakuza jinsi wanavyofanyika mifano bora na kuleta sifa kwako au kwenu. Hakuna mzazi au mlezi anayetarajia au kungojea kuaibishwa na mtoto au watoto aliowalea mwenyewe, kila mzazi hata yule asiye na uhakika wa malezi yake anatarajia mema na kuwa na ndoto njema kuhusu watoto wake.
Hatua zitakazo kusaidia
Hatua ya 1
Kamwe usiwe na upendeleo kwa yoyote, fanya kila kitu kwa usawa pasipokuonyesha upendeleo wa aina yoyote. Kumbuka kuwa kila mtoto ana vipawa au vipaji vyake vya tofauti, na uwezo wao pia hutofautiana, vyote hivi havinabudi kutambuliwa mapema utotoni na kutiwa moyo au kuhamasishwa ili kuendelea, watoto wawezeshwe kuendeleza vile wanavyoonekana kuviweza mfano kipawa cha uimbaji, akili ya ufundi, uwezo wa kimichezo nk.
Hatua ya 2
Epusha roho za mashindano baina ya watoto, ushindani mdogo mdogo na wa kawaida hauna shida kwa sababu unaweza kuchochea kujibidisha, tatitizo ni yale mashindano yanayoweza kuleta magomvi na uhasama, mara nyingi hili huonekana katika familia zenye watoto au mtoto wa baba peke yake au wamama peke yake na wale wa baba na mama (watoto wa ndoa) wanapoishi pamoja. Wakati wote ondoa tofauti baina yao katika mahusiano yao ili usije kutengeneza ndugu ambao ni maadui hata watakapo kuwa watu wazima.
Hatua ya 3
Chochea ari ya kupenda shule na utamani wa kufaulu, kila mtoto anakiwango cha juu cha uwezo ambacho kinatakiwa kutambuliwa. Kama mwanao anaonekana kukosa hamasa ya shule aliyoko jaribu shule nyingine, fanya utafiti kwa kuzungumza naye nini anachokipenda katika elimu kwasababu tafiti zinaonyesha kuwa maranyingi masuala ya shule na elimu ni maamuzi ya lazima toka kwa wazazi pekeyao pasipo watoto kuhusishwa au kushirikishwa. Jaribu nyanja mbalimbali za elimu na usikate tamaa mapema. Jitahidi kuweka akiba ya fedha kwa ajili ya elimu ya watoto wako kwasababu elimu ni bora lakini ni ya gharama, na waswahili wamesema “Ikiwa unaona elimu ni ghali basi jaribu ujinga”.
Hatua ya 4
Penda kuwa na muda na watoto wako, hususani wakati wa chakula cha jioni na zungumza nao mambo yaliyoendelea au yanayoendelea katika maisha yao kwa siku hiyo, watoto pia wanayo ya kukushirikisha, kwa namna hii watoto watafurahi na kuongeza upendo na ukaribu kwa wazazi wao. Kwa bahati mbaya tafiti zinaonyesha kuwa wazazi wa kiume hususani wakiafrika hupata nafasi marachache zaidi kula chakula cha jioni na familia zao. Ikiwa ratiba yako ya usiku haikuruhusu basi jaribu kushiriki kifungua kinywa (breakfast) pamoja na watu wengine wa familia yako. Najua wako watakaojitetea kuwa ratiba zao hazikubali kabisa ila suala ni kwamba, ukiona umuhimu wa jambo hili basi utalifanya kuwezekana.
Hatua ya 5
Kuza baadhi ya mazoea ya kifamilia yanayowaleta karibu zaidi kama vile kufanya na sherehe za krismas au pasaka au sikukuu nyingine kwa pamoja nyumbani au kusafiri pamoja wakati huo. Kukaribisha nyumbani kwenu marafiki wa mtoto au watoto wako siku za wikiendi au sikuu. Kuwaruhusu watoto kutoka kwa uangalizi maalumu. Huwezi kuelewa jinsi gani mambo haya yanaumuhimu kwa mtoto wako mpaka apate tatizo fulani ndiyo utaelewa.
Hatua ya 6
Kuwa msaada kwa watoto wako bila kujali nini kinaendelea, hata kama unavunjwa moyo na vile watoto wako wanavyoishi au tabia fulani walizonazo, waonyeshe upendo na utayari wako wa kuwasaidia, wawezeshe kufahamu jinsi gani ya kufanya vema zaidi wakati mwingine. Kamwe usiwape kisogo wanapohitaji msaada wako.
Hatua ya 7
Ruhusu watoto au mtoto wako ajue na aamini kuwa uko na utakuwepo kwa ajili yake wakati wote, wala asiwe na mashaka kabisa na hili. Najua kila familia hupitia magumu na changamoto mbalimbali katika maisha, pamoja na haya yote mruhusu ajue unampenda na utampenda daima. Hakuna kitu kibaya na kisichotoka kwa urahisi moyoni mwa mtoto kama pale mtoto anapokuwa na mashaka na malezi au ulinzi anaoupata toka kwa mzazi wake.