Ukibahatika kuoa mwanamke wa sampuli hii utayafurahia maisha. Lakini ukioa aliyejaaliwa vitu hivyo kisha akawa si muelewa wala hajui thamani ya mume na ndoa, andika maumivu. Kimsingi zipo athari nyingi za kuoa mwanamke mwenye pesa, mzuri kwa muonekano, ‘aliyebukua’ sana lakini akawa limbukeni. Leo nitagusia tatu.
Kusalitiwa kuko nje nje
Uchunguzi unaonesha kuwa, wanawake wengi malimbukeni ambao wanajijua ni wazuri na wana pesa zao wakiudhiwa kidogo tu ni wepesi kuchepuka hata kwa kuwashawishi wanaume wengine kwa pesa.
Utakuta mume kamkosea kidogo au kamkera bila kudhamiria lakini yeye anaona njia sahihi ni kutorudi nyumbani. Anaweza kwenda kulala hotelini mpaka pale mume atakapomfuata na kumpigia magoti. Wapo wanawake wa hivyo!
Ni wepesi kuomba muachane
Ukifuatilia sana wanawake wenye vigezo hivyo wanajiamini sana, hawa ndiyo wanaoongoza kwa kuomba talaka. Kosa dogo tu, atakuambia kama vipi muachane.
Anasema hivyo akijua wapo wanaume wengi wanaomsumbua na hatapungikiwa lolote. Tena hali inaweza kuwa mbaya sana kama wakati huo hamjajaaliwa mtoto kwani atajua hatakosa kitu akikuacha. Pesa anayo, ana uhakika wa kupata mwanaume mwingine fasta, kwa hiyo anaona hana cha kupoteza au kukikosa akikutosa.
Rahisi kukutawala
Chunguza sana utabaini kuwa, wanaume ambao wanasumbuliwa na wake zao wana vigezo hivyo. Baadhi ya wanawake wenye pesa na wanajijua ni wazuri wanapenda sana kuonekana wao ndiyo wenye sauti ndani ya nyumba. Watakataa kuelekezwa wala kupewa amri na wanaume zao hata kwenye masuala ya msingi. Hawa ndiyo wale ambao wanataka kurudi nyumbani muda wowote wanaotaka na wasiulizwe.
Watataka wawe wenye maamuzi ya mwisho na kila jambo la kifamilia washirikishwe laa sivyo kinanuka. Hili ni tatizo! Kimsingi ninachotaka kukifikisha kwa wanawake ni kwamba, ndoa ni heshima. Ukijaaliwa kupata mwanaume wa kukuingiza ndani, jitahidi kuithamini ndoa yako. Jua wapo wanawake wenye kila kitu lakini wamekosa wanaume wa kuwaoa na wanaitamani heshima ya ndoa.