Tuesday, April 23, 2019

Hizi ndizo sababu kuu kumi za ugumba kwa wanawake.

Hizi ndizo sababu kuu kumi za ugumba kwa wanawake.

1. Utoaji wa mimba;
Huenda hichi ndio kitakua chanzo kikuu cha ugumba miaka ijayo kwani siku hizi kila karibia kila mwanamke ana sababu za kutoa mimba, utoaji wa mimba una hatari nyingi ambazo huweza kuleta ugumba kama kuoza au kuharibika kwa kizazi baada ya kushambuliwa na bakteria, makovu yanayoletwa na vifaa vinavyotumika kutoa mimba kwenye mfuko wa uzazi na mlango wa uzazi huweza kusababisha ugumba usiotibika.

2. Matatizo ya vizaalishaji vya mayai [ovari]; 
Ovari ni kiungo ambacho kinatoa yai moja kila mwezi ili liweze kurutubishwa na mbegu ya mwanaume lakini kuna magonjwa ambayo yanaweza kusababisha ovari hiyo ikaugua na kushindwa kutoa mayai, mwanamke ana ovari mbili lakini moja ikiuugua tu na nyingine haifanyi kazi mfano ugonjwa wa ovarian cyst.

3. Matatizo ya mirija ya uzazi; 
Ovari zimeunganishwa kwenye mirija ambayo hupitisha mayai kwenda kwenye mfuko wa uzazi..Wakati mwingine mirija hiyo huziba kwa sababu mbalimbali hivyo mayai hushindwa kupita na kusababisha ugumba.Mfano ugonjwa wa endometriosis, upasuaji na peritonitis.

4. Matatizo ya kizazi; 
Kizazi ndio sehemu kuu ambayo mtoto hutunzwa na kuishi kwa miezi yote tisa, tatizo lolote linaloshambulia kizazi huleta ugumba. Mfano, makovu ndani ya kizazi, uvimbe ndani ya kizazi, kugeuka kwa kizazi na magonjwa ya zinaa kama kaswende na kadhalika.

5. Kansa; 
Kansa ya kizazi huzuia yai la mama lililorutubishwa kushindwa kujiweka kwenye kizazi ili kukua, hivyo huchangia sana mimba kuharibika au kutotungwa kabisa.

6. Matatizo ya mlango wa uzazi; 
Oparesheni za kizazi, utoaji wa mimba na magonjwa ya zinaa huweza kusababisha kuziba kwa mlango wa uzazi hivyo mbegu za kiume kushindwa kabisa kupita kwenye mlango wa uzazi na kusababisha ugumba.

7. Magonjwa mengine ya mwili; 
Magonjwa yeyote ya binadamu  ambayo huingilia mfumo wa homoni za uzazi huleta ugumba mfano magonjwa ya ini,kisukari, hyperthyrodism, na kadhalika.

8. Matumizi ya sigara na pombe;  
Unywaji wa pombe sana na uvutaji wa bangi huzuia yai kutoka kwenye ovari, lakini pia uvutaji wa sigara hupunguza uwezo wa yai kutembea kutoka kwenye ovari kwenda kwenye mfuko wa uzazi na wakati mwingine husababisha mimba kutunga nje ya kizazi.

9. Msongo mkubwa wa mawazo; 
Ukiwa unatafuta mtoto tayari ukiwa umepaniki kwamba huenda usimpate husababisha inasababisha mwili kutoa homoni kitaalamu kama cortisol ambazo huzuia kazi za homoni za uzazi kitaalamu kama gonadotrophin releasing hormone hivyo hali huzidi kua mbaya.

10. Uzito uliopitiliza; 
Mwili mkubwa unaingilia mfumo wa utengenezaji homoni za uzazi hivyo huweza kuleta ugumba katika umri mdogo sana, hivyo kupunguza uzito ni moja ya njia bora kabisa ya kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuzuia ugumba.

Mwisho.
Kabla hujaanza kuzunguka kwa waganga wa kienyeji na mahospitalini ni bora kujichunguza kama uko kwenye hatari zilizotajwa hapo juu. Hakuna dawa moja ambayo ina uwezo wa kutibu ugumba kwa watu wote bila kutibu chanzo chake kwanza.... Hivyo naweza kusema kila mtu ana dawa yake ya ugumba kulingana na historia ya maisha yake na chanzo cha tatizo lake.

Ugumba unaweza kupona kabisa kulingana na chanzo cha tatizo na hali ya ugonjwa ilivyo na unaweza usipone kabisa kama ugonjwa umeshapea sana, ndio maana kuna watu wenye uwezo mkubwa sana wa kifedha, wasanii na wafanyabishara wakubwa lakini wameshindwa kupata watoto pamoja na kwenda mpaka nje ya nchi na kuonana na madaktari bingwa kwenye hospitali za kisasa kabisa.Makala ijayo ntaongelea  matibabu ya ugumba kwa kina, usikae mbali.