Historia fupi ya maisha ya Ruge Mutahaba
Ruge Mutahaba (alizaliwa Brooklyn, New York, Marekani, 1970 - Afrika Kusini, 26 Februari 2019) alikuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Vipindi wa Clouds Media Group nchini Tanzania.Elimu
Mutahaba alipata elimu ya shule ya msingi Arusha darasa la kwanza hadi la sita, kisha akahamia Shule ya Msingi Mlimani ambako alihitimu elimu ya msingi.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Forodhani na kuhitimu kidato cha nne, na kidato cha sita katika shule ya sekondari Pugu. Alihitimu shahada ya Masoko kisha Shahada ya Sanaa katika Uchumi Chuo Kikuu cha San Jose huko California Marekani.
Taaluma
Aliporejea Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha San Jose cha California (Marekani) ambako alihitimu masomo yake, Mutahaba alianza kutambulika kwenye jamii baada ya kuanza kufanya kazi na rafiki yake Joseph Kusaga ambaye alikuwa akiendesha klabu ya usiku ya disko iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Clouds Disco.
Ushirikiano wao ulipelekea kuanzishwa kwa Clouds Media Group mjini Arusha ambayo, licha ya kuwa chombo cha habari na burudani kwa hadhira, hasa vijana, ilifanya kazi ya kuhamasisha vijana wadogo wa Kitanzania kujiingiza katika kutafuta fursa na ujasiriamali ili kujiinua na kuchangia katika maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla wake.
Familia
Vyanzo vinadai kuwa Mutahaba hakuwahi kufunga ndoa rasmi lakini alikuwa na mahusiano na Zamaradi Mketema na walipata watoto wawili.
Maradhi na sababu ya kifo
Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo Mutahaba alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo, kwa hiyo alipelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu hadi mauti yalipomfika tarehe 26 Februari 2019.
Mapokeo ya Jamii
Watanzania wengi waliopokea habari za kifo chake ikiwa ni pamoja na rais wa Jamhuri ya Tanzania John Magufuli.
Walishtushwa na habari za mauti yake na kutuma jumbe za kuguswa kutokana na mchango mkubwa wa Mutahaba katika tasnia ya habari na burudani, ubunifu katika mipango mikakati, kuendeleza vipaji vya vijana wa Kitanzania, kuhamasisha ari ya ufanyaji kazi kwa bidii katika jamii na maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.
Source: Wikipidia