Sunday, January 27, 2019

Sababu 7 za kwa nini hutakiwi kutafuta mpenzi kwenye mitandao ya kijamii

Sababu 7 za kwa nini hutakiwi kutafuta mpenzi kwenye mitandao ya kijamii 
1. Watu wanaigiza uhalisia
Katika eneo ambalo watu wanaigiza uhalisia wa maisha kwa kiasi kikubwa ni kwenye mitandao ya kutafuta wapenzi pamoja na mitandao ya kijamii.

Watu huweka picha ambazo siyo zao, majina ya uongo, maelezo binafsi ya uongo, hali za mahusiano za uongo, eneo la makazi la uongo, n.k.

Ni muhimu kuwa makini kwani nimewahi kuona watu wakikimbia baada ya kukutana na wapenzi wao wa kwenye mtandao na kubaini kuwa hawako kama walivyowafahamu au kuwatarajia.

Hivyo kutafuta mpenzi kupitia mitandao ya kutafuta wapenzi ni rahisi kutapeliwa au kudanganywa kwani watu wanaigiza uhalisia.

2. Ni biashara
Mitandao mingi ya kutafuta wapenzi imeanzishwa kwa lengo la kibiashara. Hivyo uhalisia wa kupata mpenzi sahihi ni mdogo kwani suala la kutafuta wapenzi hutumiwa kama njia ya kupata pesa.

Kwa mfano unaweza kuanza mahusiano na mtu kumbe analipwa pesa afanye hivyo ili mfumo uzidi kupata wanachama au watembeleaji zaidi na hatimae kuzalisha pesa zaidi.

Kumbuka pia baadhi ya mitandao ya kutafuta wapenzi hutoza ada ya uwanachama ili kujipatia pesa.

3. Umbali
Lengo mojawapo la mahusiano ni watu wawili kukaa pamoja kwa karibu zaidi ili washirikishane hisia zao. Hivyo kwa kiasi kikubwa umbali unaweza kuathiri mahusiano.

Pamoja na teknolojia kuwaleta watu karibu, bado kiuhalisia kuna umbali ambao hauwezi kumalizwa kwa simu au kompyuta.

Hebu fikiri haya; je unaweza kumlisha mtu kitu kwa mtandao? Je unaweza kumkumbatia mtu kwa mtandao? Je unaweza kumbusu mtu kiuhalisia kwenye mtandao? Je unaweza kumbeba mtu kwa mtandao?

Naamini umeona jisi ambavyo mtandao unafanya mahusiano yawe duni, dhaifu, yasiyo na ladha na yanayoweza kuvunjika wakati wowote.

4. Hakuna mapenzi ya kweli
Mara nyingi watu wengi wanaojiunga na mitandao ya kutafuta wapenzi ni watu wanaojaribu mifumo hiyo au watoto.

Hivyo ni vigumu sana kupata mtu mwenye nia ya dhati ya kujenga mahusiano bora ambayo hatimaye yanaweza kufikia ndoa.

Kumbuka pia kwa kuwa tovuti za kutafuta wapenzi ni nyingi, ni rahisi mtu kuvunja mahusiano kwani atapata mpenzi mwingine ndani ya muda mfupi.

5. Watu wengi wamejeruhiwa
Majeraha ya mahusiano huharibu mahusiano ya watu wengi. Tafiti mbalimbali zilibaini kuwa watu wengi wanapojeruhiwa au kukosana na wapenzi wao hukimbilia kwenye mitandao ya kutafuta wapenzi.

Hebu fikiri unaanza mahusiano na mtu mwenye majeraha na uchungu wa mahusiano yaliyopita; ni wazi hamtoweza kujenga mahusiano yatakayodumu.

6. Kudanganyana ni rahisi zaidi
Je umewahi kusikia mtu akipiga simu akiwa kwenye daladala Dar es Salaam lakini anasema yuko Mwanza? Haya ndiyo mambo yanayotawala mitandao ya kutafuta wapenzi.

Kwa kuwa humwoni mtu unayewasiliana naye, ni rahisi kukudanganya kwenye mambo mengi. Anaweza kuwa anawasiliana na wapenzi sita kwa wakati mmoja lakini hutoweza kubaini.

Hivyo mahusiano ya kawaida yaani ya ana kwa ana bado yanazidi kuwa na nguvu zaidi kuliko yale ya kwenye mtandao.

7. Unaweza kufanyiwa uhalifu
Unapoingia kwenye mahusiano na mtu kwa kupitia mitandao ya kutafuta wapenzi mnaweza kubadilishana taarifa kadhaa. Ikiwa utatoa taarifa zako muhimu kama vile pasi ya kusafiria, kadi za benki, n.k. taarifa hizo zinaweza kutumiwa na wahalifu kukufanyia uhalifu.

Kumbuka mtu anaweza kuvaa kofia ya kutafuta mpenzi kumbe ndani yake ni mwizi hatari anayetafuta kuwaibia watu; hivyo kuwa makini na mitandao hii.