Thursday, December 19, 2019

Mambo 4 ambayo wanawake wengi wanakosa kwa waume zao.

1. MPE KIPAUMBELE
Ni ukweli ulio wazi kwamba wanawake wengi wanapenda kupewa kipaumbele katika mambo yote yanayowahusu waume zao hata kama hawana uwezo wa kusaidia chochote. Kwa mfano, mwanaume anataka kununua kiwanja au nyumba kwa ajili ya kuishi yeye, mkewe na familia (kama anayo).

Ni jambo zuri kabisa analolifanya lakini mwanamke asiposhirikishwa akaja kugundua mwenyewe, atajisikia vibaya sana na huenda hata mapenzi kwa mumewe yakaanza kupungua kwa kudhani anadharauliwa.

Wanawake wengi wanapenda kushirikishwa katika kila jambo linalowahusu waume zao. Mshirikishe katika mambo madogo na makubwa hata kama unajua hawezi kuwa na msaada wowote. Ukimpa nafasi hiyo, atajiona kuwa na nafasi kubwa kwenye maisha yako na atazidi kukupenda.

2. MUUNGE MKONO
Mnapoamua kuishi pamoja, mnakuwa kama timu moja ambayo maisha yenu yanategemeana. Imekuwepo kasumba ya mfumo dume kwa kipindi kirefu, wanaume wengi wakiamini kwamba wanawake ni watu dhaifu ambao hawawezi kuwa na mchango wowote kwa familia zaidi ya kutunza nyumba na kulea watoto. Haya ni makosa makubwa wanayoyafanya wanaume.

Mkeo anapokuja na wazo kwako, muunge mkono na mtie nguvu ili aone kama anaweza kufanya mambo makubwa. Pale anapokwama mshike mkono na muoneshe njia, iwe ni kwenye biashara, kwenye kazi au kwenye mambo yake binafsi au ya familia. Muunge mkono, hiyo itasaidia sana kumfanya aone umuhimu wako na atazidi kukupenda.

3. MSIFIE MARA KWA MARA
Ni ukweli usiopingika kwamba kihaiba, wanawake ni watu wanaopenda sana kusifiwa, hasa na waume zao au watu wanaowapenda. Jenga utaratibu wa kumsifia mara kwa mara, mweleze kwamba yeye ni mzuri, ana mvuto, anapendeza akivaa nguo nzuri na vitu vya namna hiyo.

Msifie kwamba yeye ni msafi, anajua kupika, anajua kusafisha nyumba vizuri na anakuridhisha muwapo faragha. Akikufanyia mambo mazuri, mshukuru.

Huwezi kuamini kwamba kwa kufanya hivyo tu, utaweza kuuteka moyo wake kwa asilimia mia moja na ataendelea kukupenda siku zote za maisha yake. Wanaume wengi huwa na tabia ya kuwasifia wenzi wao katika siku za mwanzo za uhusiano wao lakini wakishazoeana, huacha kabisa. Usiache mkeo akasifiwe barabarani wakati wewe ndiye mwenye wajibu wa kumsifia.
Image result for black couples

4. MSIKILIZE, MPENDE
Wanawake wengi wanapenda kusikilizwa hata kama wanachokizungumza hakina maana. Anaweza kuwa anakusimulia habari za mashoga zake, watoto wa jirani au kuhusu filamu au tamthiliya anayoipenda. Msikilize na changia mazungumzo yake kuonesha mpo pamoja, hiyo itamfanya azidi kukupenda zaidi na kujisikia amani akiwa na wewe.

Baadhi ya wanaume huwa na kawaida ya kuwakatisha mazungumzo wenzi wao kwa kuona hayana maana au kuwa bize na mambo mengine, kwa mfano kuchezea simu au kuangalia TV wakati wenzi wao wakiwaongelesha.

Mwisho muoneshe kwamba unampenda na mara kwa mara mtamkie kwamba unampenda. Nakupenda ni neno dogo lakini lenye umuhimu mkubwa katika uhusiano wa watu wawili walioamua kuishi pamoja. Kubwa na muhimu zaidi, hakikisha unamridhisha muwapo faragha. Ukifanya hivyo, maumivu ya mapenzi utayasikia kwa wenzako tu.