Sababu 11 za watu wengine kutokukupenda wewe.
Kuna baadhi ya watu wanapendwa sana kwenye jamii au mazingira yanayowazunguka, kwa ujumla tunaweza kusema wanapendwa takriban na watu wote. Lakini wapo wengine wasiopendwa kabisa, na hata kama wanapendwa, basi wanapendwa na watu wachache sana.Kuishi katika jamii inayokupenda kunakufanya kuwa mwenye furaha na ufanisi katika yale unayoyafanya. Wapo baadhi ya watu wanatambua kuwa hawapendwi, lakini hawajui sababu za tatizo hilo wala njia ya kulitatua.
Ikiwa unataka kufahamu kwanini baadhi ya watu hawakupendi, basi fahamu sababu zinazosababisha watu wasikupende.
1. Siyo msikivu.
Kama unavyopenda kusikilizwa, ndivyo na watu wengine wanavyopenda kusikilizwa. Ikiwa huna muda wa kusikiliza mawazo au matatizo ya watu wengine, nao pia hawatakuwa na muda kukupenda kukusikiliza.
Epuka tabia za kutaka watu wakusikilize wewe kila wakati; tambua nawe unapaswa kuwa na muda wa kuwasikiliza.
2. Unamajivuno.
Watu wenye majivuno ni watu wabaya wanaochukiwa na kila mtu. Ikiwa unapenda majivuno, kwa hakika hutokuwa na rafiki, bali utatengwa na watu.
Tabia kama vile “nina simu kali sana”, “nina akili sana”, “nina pesa usinione hivi”, “mimi siyo wa kawaida kama nyie”, “kwetu mambo safi”, “wewe huna hadhi yangu”, n.k. ni baadhi ya tabia mbaya za majivuno.
Ikiwa unatamani watu wakupende na wawe karibu nawe, acha tabia ya kujivuna na kujikweza.
3. Mbinafsi.
Ubinafsi ni tabia mbaya ya kujijali wewe pekeyako na mambo yako. Hakuna mtu atakayekupenda ikiwa wewe ni mtu unayejali tu mambo yako binafsi. Ni lazima wakati mwingine uthamini na kujali maisha na mambo ya watu wengine.
4. Unaupendeleo.
Mtu mwenye upendeleo huchukiwa na watu kwa kuwa anagawa watu kwenye makundi. Mtu mwenye upendeleo huwa na watu wanaotakiwa kupata zaidi na wengine wanaotakiwa kupata kidogo.
Haki ni msingi wa kuishi na watu vizuri; ikiwa unatabia ya kupendelea watu kwa kuwa ni ndugu, marafiki, dini moja au kabila moja, basi acha tabia hiyo mara moja kwani itakufanya uchukiwe na watu.
5. Unazungumza na watu ukiwa na shida.
Inawezekana huwasalimii hata watu wengine, unakutana na mtu unapishana naye kama gogo. Ukiwa na shida unaanza kujikombakomba kwa watu ili wakusaidie.
Ikiwa unataka kupendwa na watu, ni muhimu kuzungumza na watu wengine kila wakati hata kama huna shida. Hili litakujengea msingi mzuri wa mahusiano katika maisha yako.
6. Mmbea na msengenyaji.
Nawachukia sana watu wambea na wasengenyaji, kwani mtu mmbea akiwa na wewe anakueleza mambo ya mwingine na akiwa na mwingine anamweleza mambo yako.
Ikiwa unapenda umbea na kusengenya wengine basi acha tabia hiyo mara moja. Kueneza umbea na kuwasengenya watu wengine kutakufanya uchukiwe na utengwe na watu.
7. Unalaumu sana wengine
Inawezekana kila kitu kinachoharibika kwenye maisha yako wewe unalaumu, tena unalaumu watu wengine. Kwa hakika usipoacha tabia ya kulaumu watu wengine juu ya matatizo yanayokukabili hakuna mtu atakayekupenda.
8. Siyo mtoaji.
“Mchoyo hana rafiki.”
Kwa kawaida watu humpenda mtu anayetoa. Siyo lazima utoe mamilioni, kutoa hata soda moja au kumlipia mtu nauli ya daladala kuna maana kubwa.
Ikiwa unataka kupendwa na watu basi acha tabia ya uchoyo leo.
9. Mwongo.
Mtu mwongo ni hatari. Hakuna mtu anayependa kukaa na mtu mwongo.
Unachukua kitu unasema siyo wewe, unafanya kitu unasema siyo wewe, unakwenda mahali unadanganya, n.k. Je unafikiri kuna mtu atakuamini na kukupenda? Acha tabia ya uongo ili upendwe na kuaminika.
10. Huna maadili mema.
Unavaa hovyo, unanyoa nywele hovyo, unapenda ulevi na uzinzi, mvivu, n.k. Je unafikiri kuna mtu atakayekupenda?
Watu wanapenda kukaa na watu wenye maadili mema; usipoacha tabia mbaya utaishia kukaa na wahuni wenzako na hakuna mtu wa maana atakayekuthamini.
11. Unazungumza bila utaratibu.
Hekima ya kutawala kinywa chako ni muhimu sana katika kupendwa na watu. Inawezekana unazungumza hovyo mbele ya watu wa heshima, unapayuka barabarani bila sababu, mtukanaji, unaimba na kuzungumza mambo machafu n.k.
Kwa hakika tabia kama hizi zitafanya watu wakuchukie na kukutenga. Tawala kinywa chako, fahamu unazungumza nini kwa ajili ya nini na wapi.
Pasipo shaka umebaini wazi kuwa ni kwanini watu hawakupendi. Hivyo basi, kuacha tabia tajwa hapa juu pamoja na nyingine zinazoendana na hizi kutakufanya ukubalike, uthaminike na upendwe na watu wengi zaidi.