Saturday, February 9, 2019

Faida 10 za kuachana na uvutaji wa sigara

Faida 10 za kuachana na uvutaji wa sigara
1. Unaokoa pesa
Moja kati ya mambo yanayowapotezea watu pesa ni tabia kama vile uvutaji wa sigara.

Kwa kuacha kuvuta sigara utaweza kuokoa pesa ambazo huwa unazitumia kwa ajili ya kununua sigara, na kuzitumia kufanya mambo mengine yenye manufaa kwako.

2. Unarudisha afya yako
Uvutaji wa sigara huathiri afya ya mwanadamu kwa namna mbalimbali. Hivyo kuacha kuvuta sigara kutakuepusha na maradhi kama vile shambulio la moyo, saratani ya mapafu, kuzeeka kwa ngozi, matatizo ya ubongo, n.k.

3. Utaishi muda mrefu
Nicotine inayopatikana kwenye sigara huathiri mishipa ya damu kwa kuifanya iwe miyembamba na kusababisha damu kutokupita vizuri.

Ikiwa damu haitasafiri sawasawa, sehemu za mwili kama vile ubongo utakosa kiwango cha kutosha cha damu, jambo linaloweza kusababisha kiharusi na hatimaye kifo.

4. Unalala vizuri
Ikizingatiwa kuwa nicotine ni kichochezi (stimulant) ambacho hufanya ubongo wako kutokutulia na kukuruhusu kulala vyema.

Hivyo kuacha uvutaji wa sigara kutakuwezesha kupata usingizi mzuri na hatimaye kuwa na afya njema.

5. Unapona vidonda mapema
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na chuo Kikuu cha Washington mwaka 2007, unaeleza kuwa uvutaji wa sigara huchelewesha kwa kiasi kikubwa kupona majeraha ya vidonda.

Hivyo hakuna haja ya kuvuruga mchakato wa wewe kupona majeraha kwa sababu ya kutumia sigara.

6. Unaweza kujitawala
Sigara hukufanya kuwa mtawaliwa (addicted). Mara nyingi mtu anayevuta sigara hushindwa kujitawala, anaweza kuvuta hata usiku wa manane, hosipitalini, maeneo yenye mikusanyiko, n.k. bila kuweza kujizuia.

Hivyo kuacha sigara hukufanya uweze kujitawala tena na si kutawaliwa na sigara.

7. Unalinda wanaokuzunguka
Moshi wa sigara una zaidi ya kemikali 4,000 na 43 kati yake zinafahamika wazi kusababisha saratani za aina mbalimbali. Hivyo uvutaji wa sigara haukuathiri tu wewe bali hata wale wanaokuzunguka, hasa wanafamilia.

Kuacha sigara kutalinda afya yako na wale wanaokuzunguka kwa ujumla.

8. Unalinda afya ya akili
Uchunguzi uliofanyika mwaka 2010 kwa watu wenye umri mkubwa ambao walikuwa wavutaji wa sigara, ulibaini kuwa walikabiliwa na matatizo ya akili kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wale wasiovuta sigara.

Kutokana na utafiti huu ni ukweli kuwa uvutaji wa sigara huathiri afya ya ubongo na hatimaye kupelekea matatizo ya akili.

9. Unalinda afya ya uzazi
Utafiti uliofanyika mnamo mwaka 2007 ulibaini kuwa uvutaji wa sigara una athari kubwa kwenye afya ya uzazi ya mwanaume na mwanamke pia.

Inaelezwa kuwa sigara huharibu mbegu za kiume, husababisha kutoka kwa mimba, huharibu mayai ya uzazi ya wanawake pamoja na kuathiri viungo vya uzazi kwa ujumla. Hivyo kuacha sigara ni kulinda afya yako ya uzazi.

10. Unaondoa harufu mbaya
Watu wanaovuta sigara wamekuwa wakiwakera watu wengi kutokana na harufu mbaya inayotokana na uvutaji wa sigara. Wengine wamekuwa wakitumia dawa mbalimbali ili kukabili harufu hiyo bila mafanikio.


Kwa hakika suluhisho la uhakika la kukabili harufu mbaya ya sigara ni kwa kuacha kuvuta sigara pekee na si vinginevyo.