Mwanamuziki nguli Oliver Mtukudzi amefariki dunia
Mwanamuziki nguli kutoka nchini Zimbabwe Oliver Mtukudzi amefariki dunia. Amefariki hii leo katika hospitali ya Avenues mjini Harare.Mtukudzi amekuwa akiugua kwa muda sasa. Alilazimika kukatiza miadi kadhaa katika fani hiyo ya muziki katika mataifa mbali mbali duniani kutokana na kuugua kwake.
Muziki wake wa mtindo wa afro-jazz ulivuka mipaka na kupata mashabiki wengi kote duniani.
Alipata umaarufu nchini Zimbabwe kabla ya nchi hiyo kupata uhuru mnamo 1980 alipojiunga katika jeshi na muimbaji mwenza wa Zimbabwe anayeishi Marekani, Thomas Mapfumo kutoa sauti ya mapinduzi katika wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa inakabiliana na serikali ya Ian Smith.
Baada ya uhuru wa nchi hiyo, aliitumia sauti yake kuzungumzia masuala ya kisiasa na ya kijamii. Kwa mara nyingi ujumbe ndani ya muziki wake ulikuwa ni wa ndani kukwepa mkono wa serikali iliyokuwa haipendelei kukosolewa.
Mtukudzi amekuwa katika taaluma ya muziki kwa zaidi ya miongo minne, na amefanikiwa kutoa albamu 67. Albamu yake ya mwisho imeangazia hali ya kisiasa hivi sasa Zimbabwe na matatizo ya kijamii.
Nyota huyo wa muziki kutoka Zimbabwe alikuwa anapewa heshima ya muziki wa Afrika kama ilivyo kwa wasanii kama Hugh Masekela, Steve Dyer, Miriam Makeba, Yousssou N dour, Angelique Kidjo, Yvonne Chaka Chaka na Lady Smith Black Mambazo.