Friday, December 20, 2019

Jua jinsi ya kumdhibiti mpenzi anayepiga mizinga

MWELEZE UKWELI
Kama huna pesa wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile. Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana pesa au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ?mizinga? ili afaidi.

Ishi kawaida, kuwa mkweli kwake siku zote, utakapokuwa mkweli kwake atakuheshimu kwa uwazi wako. Siku zote zilingane, uwe una fedha au huna asijue, hilo litakusaidia kwa kiwango kikubwa sana katika maisha yako ya kimapenzi.

JENGA MAZINGIRA YA YEYE KUKUSAIDIA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa! Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya daladala analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake. Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.

BANA MATUMIZI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo! Wakati akiwa anaamini hivyo, ukweli ulionao moyoni ni kwamba huna fedha za kutosha.

Unachotakiwa kufanya mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakusababishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.

Kwa kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, mapenzi ni kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku moja na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga 'mizinga' mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.