Thursday, April 18, 2019

Sifa 10 ambazo kila mjasiriamali anatakiwa kuwa nazo

Sifa 10 ambazo kila mjasiriamali anatakiwa kuwa nazo
1. Mwenye malengo
Malengo ni mwongozo wa kukuwezesha kufanikisha jambo lolote. Kuwa na malengo ni sifa muhimu ambayo kila mjasiriamali anapaswa kuwa nayo. Je umeamua kuwa mjasiriamali kwenye nini? Kwa ajili ya nini?

Malengo yatakuongoza ufanye nini, wapi lini na kwa ajili ya nini. Bila malengo utafanya mambo bila mwongozo wowote na ni vigumu kufanikiwa.

2. Nidhamu
Nidhamu ni sifa muhimu kwa mjasiriamali kwani itamtenga na mambo mengi yasiyokuwa na umuhimu. Ni lazima mjasiriamali awe na nidhamu ya maswala kama vile matumizi ya muda pamoja na pesa.

Kila mjasiriamali anapaswa kujinyima na kukataa vitu vyote ambavyo havimwezeshi kufikia malengo yake.

3. Ujasiri na uthubutu
Ujasiri na uthubutu ni sifa muhimu sana kwa mjasirimali ili aweze kutekeleza malengo yake. Ujasiriamali ni swala linalohitaji ujasiri na uthubutu wa kuchukua maamuzi magumu hata kama kuna changamoto au hatari kadha wa kadha.

Huwezi kuwekeza pesa zako kwenye mradi au biashara yoyote kama hutokuwa na ujasiri na uthubutu. Ujasiri na uthubutu hautaruhusu hofu na mashaka ya kushindwa au kupata hasara vikutawale.

4. Ubunifu
Ubunifu humtofautisha mjasiriamali mmoja na mwingine. Unahitaji ubunifu ili ubuni wazo la pekee ambalo litakupa matokeo mazuri. Wajasiriamali wengi hawana ubunifu ndiyo maana wanakwama.

Kwa mfano mjasiriamali mmoja akianzisha biashara ya kuuza maandazi, basi wengine 20 wataiga. Ni lazima mjasiriamali uwe na ubunifu utakaokuwezesha kufanya mambo yenye tija.

5. Uvumilivu
Kila jambo lina changamoto zake. Ujasiriamali una changamoto nyingi ambazo zinahitaji uvumilivu ili kuzimudu.

Hivyo basi, sifa ya kuwa na uvumilivu ni muhimu sana kwa kila mjasiriamali anayetaka kufanikiwa. Haijalishi umepata hasara au unakutana na changamoto nyingi kiasi gani, ni muhimu kuvumilia.

6. Bidii
“Mafanikio huja kwa wale ambao wanafanya bidii kubwa kuyatafuta.” - Henry David Thoreau

Bidii ni msingi wa kufanikiwa kwenye jambo au shughuli yoyote. Ni muhimu kukumbuka kuwa mjasiriamali ni mwajiri (boss) wake yeye mwenyewe. Hivyo ni muhimu kujituma na kufanya kazi kwa bidii bila kusukumwa na mtu yeyote.

7. Kupenda anachokifanya
“Fanya unachokipenda na pesa zitafuata.” Marsha Sinetar

Watu waliofanikiwa sana duniani, wanafanya kile wanachokipenda. Unapofanya kile unachokipenda ni rahisi kufanikiwa kwani utakifanya kwa moyo, bidii pamoja na kutokata tamaa.

Kila mjasiriamali anatakiwa kuhakikisha kuwa anafanya kitu anachokipenda ili aweze kufikia malengo yake.

8. Kuishi na watu vizuri
Kila mjasiriamali anahitaji watu wengine ili kufanikisha malengo yake ya ujasiriamali. Kuishi na watu vizuri ni sifa muhimu kwa mjasiriamali kwani itamjengea soko zuri pamoja na nguvu kazi bora.

Hakuna haja ya kudharau au kutenga watu bila sababu. Usijenge chuki au ugomvi usiokuwa na sababu kati yako na watu wengine. Kumbuka kuwa watu ndio chanzo na msingi wako wa kupata faida.

9. Mwenye kupenda kujifunza na mtafiti
Katika swala zima la ujasiriamali, kutafiti na kupenda kujifunza ni tabia muhimu sana. Kila mjasiriamali anatakiwa kuwa na sifa hii ili aweze kujifunza na kutafiti njia na mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kumfanya mwenye tija zaidi.

Ni muhimu kukumbuka kuwa kuna wakati mjasiriamali anatakiwa kukaa chini kutafiti na kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatamwezesha kufanikiwa kwenye kile anachokifanya.

10. Kujifunza kutokana na makosa
Kama ulivyowahi kusikia mara kadhaa kuwa makosa ni shule muhimu kwa kila mtu, ndivyo ilivyo pia kwa mjasiriamali.

Mjasiriamali anapaswa kuwa na sifa ya kupenda kujifunza kutokana na makosa ili asiyarudie tena mbeleni na wala si kuyaogopa au kuyakimbia.

Kama uliwekeza pesa zako zikapotea, basi usiache ujasiriamali bali baini ni nini kilisababisha ukapoteza pesa zako ili ukiepuke mbeleni.