Thursday, January 24, 2019

Tabia 10 za msingi zitakazobadili maisha yako kabisa.

Tabia 10 za msingi zitakazobadilisha maisha yako kabisa
1. Epuka marafiki au watu wasiofaa
Wahenga walisema “ndege wanaofanana huruka pamoja”. Je kwanini ukae na watu wavivu au wazembe kama wewe huna tabia hizo au zingine zinazofanana na hizo? Jijengee tabia ya kuwaepuka marafiki au watu wasiofaa katika maisha yako kwani hawatakusaidia kufikia malengo yako bali watakudidimiza.

Tafuta watu ambao watakutia moyo na kukupa hamasa ya kutimiza malengo yako. Hata kama ni watu mnaopendana kiasi gani, kama hawana tabia zinazofaa basi ni bora uwaepuke.

2. Jifunze kuridhika
Je umewawahi kufikiri labda ukiwa na trilioni mia moja kwenye akaunti yako ndipo utakaporidhika? Kama jibu ni ndiyo basi unakosea. Usipokuwa na uwezo wa kuridhika na ulicho nacho hutaweza kuwa na utulivu katika fikra zako hata kama utapata vitu vingi kiasi gani.

Nikukumbushe kuwa simaanishi uridhike na hali mbaya uliyonayo kwa kutojishughulisha kuiboresha bali jitahidi kuepuka tamaa zisizo na masingi. Jifunze kuwa maisha yana hatua mbalimbali ambazo nyingine ni duni na nyingine ni bora.

Ukijizoeza kuwa na tabia ya kuridhika utayabadili na kuyaboresha maisha yako hatua kwa hatua.

3. Pata muda wa kutosha wa kupumzika
Kufanikiwa katika maisha au kufikia malengo yako si kutopumzika. Umewahi kufikiri usipolala au kupumzika kwa namna moja au nyingine ndipo utakapo badili maisha yako? Tafadhali usiwaze hivi tena, kwani ili uwe mtu mwenye ufanisi unahitaji muda wa kutosha wa kupumzika ili kuufanya mwili wako kuwa wenye afya njema.

Epuka tabia za kutumia simu na mitandao ya kijamii wakati wa kumpumzika hasa wakati wa kulala. Wengi hupenda kulala saa nane usiku kutokana na matumzi ya simu na mitandao. Jambo hili limewafanya wengi kuamka wachovu hivyo kushindwa kufanya kazi za siku sawasawa.

4. Tekeleza mambo hata kama utakwama
Watu waliofanikiwa duniani ni wale waliopata mawazo na kuyafanyia kazi bila kuogopa kuwa watakwama au la. Epuka tabia ya woga na kulalamika. Jifunze kufanyia kazi mawazo uliyonayo ili uweze kuona matokeo yake katika maisha.

Kama una wazo la biashara au ujasiriamali mwingine anza kulitekeleza leo. Kama una woga sana anza taratibu; unaweza ukaanza kwa kuuza hataa vitu 20 – 50 kama unaogopa kuwa na vitu vingi mwanzoni. Usiogope kuhusu mtaji; anza na mtaji ulionao hata kama ni elfu kumi kwani utaendelea kukua taratibu.

5. Tunza muda
Mambo yote tuyafanyayo hufungwa katika muda; mambo tuliyonayo ni mengi sana hivyo unahitajika kutunza muda vyema. Jifunze kujiwekea ratiba na kuifuata kila siku. Epuka mambo yasiyokuwa ya lazima kwenye muda wako.

Badala ya kutumia saa 6 kuangalia filamu, kucheza gemu au kutumia mitandao ya kijamii tumia muda huo kufanya vitu vingine vyenye tija zaidi. Unaweza kufanya shughuli nyingine mbadala kama vile ubunifu; kusoma vitabu, kujifunza maarifa mapya usiyokuwa nayo, kilimo cha bustani n.k.

6. Jikite kwenye malengo yako
Je una malengo binafsi? Je unafanya bidii kuyafikia? Je umeshayatimiza? Kama huna malengo na hujaanza kuyafanyia kazi, basi unatakiwa kuchukua hatua mapema. Malengo yatakuongoza kujua unaelekea wapi na kuwa nani katika maisha maisha yako.

Kama wewe unataka kuwa na kiwanda cha kutengeneza nguo ni lazima ujue ni hatua zipi stahiki za kuchukua ili kukamilisha lengo lako.

Mambo yatakayokuwezesha kutimiza malengo yako

  • Jipatie maarifa stahiki.
  • Jifunze kutunza fedha.
  • Tunza muda.
  • Jenga udhubutu.


7. Jifunze kusema hapana
Hapana ni jibu rahisi pia dogo sana lakini lina nguvu kubwa. Usikubali kuwa mtu anayepokea na kukubaliana na kila kitu. Twende sokoni, unaenda; twende disko, unaenda; kunywa pombe, unakunywa; nakupenda, unakubali; twende tukatembee unaenda.

Jifunze kusema hapana hata kama hutamfurahisha unayempa jibu hilo. Tabia hii litakuepusha na mipango isiyo sahihi au ya lazima katika maisha yako. Jitahidi kujenga tabia ya kukubali na kufuata yale yanayolenga kukuwezesha kuyafikia malengo yako.

8. Bainisha mambo yaliyo na kipaumbele kwako
Kuna mambo mengi ya muhimu kwako lakini baadhi ni muhimu zaidi. Hakuna haja ya kutumia kila pesa unayoipata kwa ajili ya vitu kama vile simu, nguo, viatu, au vyakula vya bei kubwa wakati huna uwekezaji wowote wa uhakika unaokuza kipato chako.

Hakikisha unajijengea tabia ya kubainisha mambo yaliyo na kipaumbele kwako na kuyafanyia kazi. Kila siku itokayo kwa Mungu hakikisha unafanya kitu katika kusogelea au kutimiza ndoto zako.

9. Jifunzae kutunza fedha
Kutafuta pesa ni jambo moja na kuzitumia vyema ni jambo lingine. Wapo watu wanaopata pesa nyingi sana lakini kwa kutokuwa na uelewa juu ya utunzaji wa pesa haziwasaidii. Kama nilivosema kwenye hoja iliyopita, yakupasa kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.

Upatapo pesa hakikisha unaweka akiba kwa ajili ya wakati ujao. Ni vyema pia kuwaza juu ya nini na niwapi uwekeze pesa zako badala ni nini huna au ni wapi utumie pesa zako. Ukiwa na tabia ya kutunza pesa utaboresha maisha yako kwani hata wakati huna kipato utakuwa na akiba yakutosha.

10. Ongeza maarifa kila wakati.
Watu wengi ni wavivu kusoma, hasa mambo ambayo si ya kustarehesha. Huwezi kubadili maisha yako kama hutakuwa na tabia ya kuongeza maarifa yako kila wakati. Jitahidi kusoma vitabu, sikiliza na tazama video zenye kukuza maarifa pia soma tovuti mbalimbali zitakazopanua maarifa yako.

Tafuta tovuti au vitabu vinavyoendana na malengo na maono yako; hivi vitakupa hamasa, mwanga na mwongozo wa jinsi ya kufikia malengo yako. Usisahau pia kusoma vitabu na habari mbalimbali zihusuzo watu waliofanikiwa kama vile Bill Gates, Warren Buffet Mark Zuckerberg na wengine wengi.